Walimu wa Kanisa wa kwanza kutangazwa walivyochorwa na Pier Francesco Sacchi mwaka 1516 hivi. Kwa sasa mchoro unatunzwa huko Paris , Ufaransa . Kuanzia kushoto mbele: Agostino wa Hippo , Papa Gregori I , Jeromu na Ambrosi wa Milano .Mwalimu wa Kanisa ni jina la heshima ambalo kwa nadra Kanisa Katoliki linampa mtakatifu ambaye katika maisha, mafundisho na maandishi yake alionyesha na kueneza mwanga wa pekee katika masuala ya imani , maadili na maisha ya kiroho .
“Tamko la kwamba mtakatifu fulani ni Mwalimu wa Kanisa lote linategemea utambuzi wa karama maalumu ya hekima ambayo alijaliwa na Roho Mtakatifu kwa faida ya Kanisa ikabainishwa na athari njema ya mafundisho yake katika Taifa la Mungu ” (Papa Benedikto XVI , Barua ya Kitume ya tarehe 7 Oktoba 2012 ).
Utaratibu
Jina hilo linatolewa na Papa au Mtaguso . Mpaka sasa, katika miaka karibu 2000 ya historia ya Kanisa wanaume 32 na wanawake 4 tu wamepewa heshima hiyo.
Wa kwanza kutangazwa (mwaka 1298 ) ni mababu wa Kanisa wanne muhimu zaidi upande wa Magharibi: Ambrosi wa Milano , Agostino wa Hippo , Jeromu na papa Gregori I .
Mwaka 1568 walitangazwa mababu wa Kanisa wanne muhimu zaidi upande wa Ukristo wa Mashariki : Atanasi wa Aleksandria , Basili Mkuu , Gregori wa Nazienzi na Yohane Krisostomo , pamoja na Thoma wa Akwino , mwalimu bora wa Karne za Kati upande wa Ukristo wa Magharibi .
Halafu mapapa wakaendelea kuongeza wengine. Wa mwisho kutangazwa kwa sasa ni Gregori wa Narek (12 Aprili 2015 ).
Orodha
Mwaka wa kutangazwa ukifuatwa na nyota unaonyesha watakatifu wanaoheshimiwa na Waorthodoksi pia, ingawa kwao hakuna cheo cha mwalimu wa Kanisa.
Papa Gregori I (540 hivi - 604 ) - 1298 *
Ambrosi wa Milano (340 hivi - 397 ) - 1298 *
Agostino wa Hippo , Doctor Gratiae (354 - 430 ) - 1298 *
Jeromu (347 - 420 ) - 1298 *
Yohane Krisostomo (347 hivi - 407 ) - 1568 *
Basili Mkuu (329 hivi- 379 ) - 1568 *
Gregori wa Nazianzo (329 - 390 hivi) - 1568 *
Atanasi wa Aleksandria (295 hivi - 373 ) - 1568 *
Thoma wa Akwino , Doctor Angelicus au Doctor Communis (1225 hivi - 1274 ) - 1568
Bonaventura wa Bagnoregio , Doctor Seraphicus (1217 hivi - 1274 ) - 1588
Anselm wa Canterbury , Doctor Magnificus (1033 hivi - 1109 ) - 1720
Isidori wa Sevilia (560 - 636 ) - 1722 *
Petro Krisologo (380 hivi - 450 hivi) - 1729 *
Papa Leo I (400 hivi - 461 ) - 1754 *
Petro Damiani (1007 - 1072 ) - 1828
Bernardo wa Clairvaux , Doctor Mellifluus - (1090 - 1153 ) - 1830
Hilari wa Poitiers (315 hivi - 367 ) - 1851 *
Alfonso Maria wa Liguori , Doctor Zelantissimus (1696 - 1787 ) - 1871
Fransisko wa Sales , Doctor Caritatis - (1567 - 1622 ) - 1877
Sirili wa Aleksandria , Doctor Incarnationis (370 hivi - 444 ) - 1883 *
Sirili wa Yerusalemu (315 - 386 hivi) - 1883 *
Yohane wa Damasko (676 hivi - 749 hivi) - 1883 *
Beda Mheshimiwa (672 hivi - 735 ) - 1899 *
Efrem Mshamu (306 hivi - 373 ) - 1920 *
Petro Kanisi (1521 - 1597 ) - 1925
Yohane wa Msalaba , Doctor Mysticus (1542 - 1591 ) - 1926
Roberto Bellarmino (1542 - 1621 ) - 1931
Alberto Mkuu , Doctor Universalis (1205 hivi - 1280 ) - 1931
Antoni wa Padua , Doctor Evangelicus (1195 - 1231 ) - 1946
Laurenti wa Brindisi , Doctor Apostolicus (1559 – 1619 ) - 1959
Teresa wa Yesu (1515 - 1582 ) - 1970
Katerina wa Siena (1347 - 1380 ) - 1970
Teresa wa Mtoto Yesu , Doctrix Amoris (1873 - 1897 ) - 1997
Yohane wa Avila (1500 hivi - 1569 ) - 2012
Hildegarda wa Bingen (1098 hivi - 1179 ) - 2012
Gregori wa Narek (951 hivi - 1003 hivi) - 2015 *
Irenei wa Lyon , Doctor Unitatis (130 hivi - 202 ) - 2022