Paralaksi inasababisha nyota (njano) kuonekana mahali tofauti ikipimwa kutoka sehemu mbili tofauti za obiti ya Dunia


Parsek (en:parsec, kifupi cha parallax second, kutoka maneno paralaksi na sekunde) ni kipimo cha umbali kinachotumiwa katika astronomia kwa kutaja umbali kati ya nyota na violwa vingine vya angani. Kifupi chake ni pc.

Umbali wa parsek 1 ni sawa na miakanuru 3.26 au karibu kilomita trilioni 31 au mita 3.0857×1016.

Ufafanuzi wa parsec ni umbali kati ya Jua na gimba la angani linaoonekana kwa pembe la paralaksi la sekunde moja ya tao (en:arcsecond).

Msingi wa kipimo hiki ni hali ya paralaksi inayosababisha ya kwamba nyota inaonekana mahali tofauti kama inaangaliwa kutoka sehemu moja kwenye obiti ya Dunia ikizunguka Jua au kutoka sehemu nyingine kinyume chake. Tofauti hii ilhali umbali wa Jua-Dunia unajulikana inaruhusu kupiga hesabu ya trigonometria na kugundua umbali wa nyota iliyopimwa.

Kwa kutaja umbali mkubwa sana kuna pia vizio vya kiloparsek (kpc), megaparsek (Mpc) na gigaparsek (Gpc).

Wanaastronomia hupendelea kutaja umbali kwa parsek kuliko miakanuru.

Parsek na Kiloparsek

Umbali kati ya nyota jirani hutajwa kwa Parsek. Kama umbali unazidi parsek 1,000 kizio cha Kiloparsek kinatumiwa, kwa mfano kutaja umbali kati ya sehemu tofauti ya galaksi moja au ndani ya kundi la galaksi.

Megaparsek na gigaparsek

Umbali wa milioni moja parsek huitwa Megaparsek (Mpc). Umbali kati ya galaksi au kati ya makundi ya galaksi hutajwa kwa megaparsek. Zaidi ya megaparsek 1,000 hutajwa kwa Gigaparsek (Gpc). Gigaparsek 1 inalingana na miakanuru bilioni 3.26

Mifano

Tanbihi

  1. The ACS Virgo Cluster Survey. XIII. SBF Distance Catalog and the Three-dimensional Structure of the Virgo Cluster, tovuti ya Chuo kikuu cha Harvard, iliangaliwa julai 2017
  2. Misconceptions about the Big Bang, tovuti ya Scientific American March 2005, kupitia tovuti ya archive.org, ilitazamiwa Julai 2017